Ticker

6/recent/ticker-posts

Kukua kwa Gospel live recording ni faida au gharama Kubwa?

                    Mwimbaji wa Injili Dr Ipyana, akihudumu kwenye moja ya maonyesho yake.


Tanzania inashuhudia ongezeko kubwa la wasanii wa muziki wa injili wanaofanya live recording badala ya studio albums, huku sababu kubwa ikiwa ni mapinduzi ya kiteknolojia yanayoboresha ubora wa sauti. Hata hivyo, pamoja na ukuaji huu wa live recording, bado kuna mjadala kuhusu faida na changamoto zinazowakabili wasanii wa injili nchini.


Katika mazungumzo na mtandao wa Gospel Connect TZ, mwimbaji wa injili Minister Mikaya Kabuka alieleza kuwa maendeleo ya teknolojia na uwepo wa wahandisi wa sauti wenye ujuzi yamewafanya wasanii wengi kuwa na hamasa ya kufanya live recording. “Faida kubwa ni kuunganisha msanii moja kwa moja na watu anaowahudumia, kuwa na ubora wa sauti wa hali ya juu, na uwezo wa kurekodi audio na video kwa wakati mmoja,” alisema Minister Mikaya.



                 

                   Minister Mikaya Kabuka akihudumu.

Hata hivyo, licha ya manufaa haya, bado kuna changamoto kubwa za kiuchumi zinazokumba wasanii wa injili wanaoamua kufanya live recording. Gharama za kukodi ukumbi wa kisasa, vifaa vya sauti vya hali ya juu, wahandisi wa sauti, waandaaji wa muziki, na waimbaji wa nyuma ni kubwa ikilinganishwa na njia ya zamani ya kurekodi studio albums. Pia, wasanii wengi bado wanakabiliwa na changamoto ya kurejesha gharama walizotumia, kwani soko la muziki wa injili Tanzania bado halijafikia kiwango cha kimataifa ambapo live recordings huleta mapato makubwa kupitia mauzo na hakimiliki.


Kwa mujibu wa wachambuzi wa muziki wa injili, faida nyingine ya live recording ni kwamba inawasaidia wasanii kujenga chapa yao (brand) kwa hadhira kubwa zaidi, kwa kuwa wanapata fursa ya kuonyesha vipaji vyao vya moja kwa moja bila urekebishaji wa studio. Aidha, video za live recording zinapendwa zaidi na watazamaji kwenye majukwaa ya kidijitali kama YouTube, Facebook, na TikTok, hivyo kuongeza uwezekano wa kufikia mashabiki wengi zaidi.


Kwa upande mwingine, changamoto kuu ni kuwa si kila msanii anaweza kumudu gharama za live recording, na wengi wao hulazimika kutegemea wadhamini au michango ya waumini ili kufanikisha miradi yao. Pia, ukosefu wa mfumo thabiti wa usambazaji wa kazi za muziki wa injili na miundombinu dhaifu ya hakimiliki inafanya iwe vigumu kwa wasanii kurejesha gharama zao.


Licha ya changamoto hizi, Minister Mikaya anaamini kuwa mabadiliko haya ya kiteknolojia ni muhimu kwa maendeleo ya muziki wa injili Tanzania. “Ingawa bado hatujafikia viwango vya kimataifa, naamini tutaendelea kusonga mbele na hatimaye kufikia malengo yetu,” alisema.

Kwa sasa, swali linalobaki ni ikiwa wasanii wa injili nchini wataweza kupata faida ya kiuchumi kutokana na live recording, au kama wataendelea kukabiliana na changamoto za kifedha katika harakati za kufanikisha kazi zao.

 

Post a Comment

0 Comments